Mkutano Simba wapingwa

Image result for simba sport club
BARAZA la Wadhamini wa Simba limemwomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kusimamisha mkutano wa dharura wa mabadiliko ya Katiba uliopangwa kufanyika Desemba 11 kutokana na wao kutoshirikishwa chochote kama wenye mali.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa baraza hilo, Hamisi Kilomoni alipozungumza na waandishi wa habari jana akisema inaweza kuleta mpasuko ambao utakuwa na madhara kiusalama.
“Mkutano uliopita mliona Mwenyekiti Aveva akitolewa chini ya usalama wa askari hali iliyoonesha kuwa usalama ulikuwa mdogo, hivyo tunaomba mkutano wa Desemba 11, usifanyike hadi wanachama wahakikiwe,” alisema Mzee Kilomoni.
Pia Kilomoni alisema wamepokea barua kutoka kwa wanachama wakilalamikia mkutano huo ambapo nakala za barua zimefika hadi kwa Rais John Magufuli, Waziri Mkuu, Waziri wa Michezo, Baraza la Michezo (BMT) pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hivyo kwa kuangalia kwa kina wanaiomba Serikali kusimamisha mkutano huo.
“Hapa kuna barua nyingi kutoka kwa wanachama kuomba kusitisha mkutano huo, mpaka kufikia kupeleka barua kwa Rais wa nchi ujue hilo sio suala dogo sisi kama wenye klabu tumeamua kumuomba Mkuu wa mkoa kuusimamisha ili isije ikatokea balaa zaidi,” alisema Kilomoni.
Aidha, Mzee Kilomoni alisema bado yeye yupo kwenye orodha ya wadhamini wanne wa klabu hiyo baada ya kupinga kuenguliwa kwenye mkutano mkuu wa wanachama uliofanyika Agosti mwaka 2014.
Kilomoni alithibitisha kwa kuonesha barua kutoka Rita iliyotolewa Agosti 12 mwaka huu ikianisha majina ya wadhamini wa klabu ya Simba, ambao ni Abdul Wahab Abas, Ally Sykes (marehemu), Ramesh Patel na yeye mwenyewe (Kilomoni).
Mkutano huo utakaofanyika Jumapili ijayo ni kwa ajii ya kupitisha mabadiliko ya Katiba ya Simba ili iweze kukidhi mchakato wa ubadilishaji umiliki wa klabu hiyo unaotaka kufanywa na mdau wa Simba Mohamed Dewji.
Tayari Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupitia katibu wake Mohamed Kiganja ilishazuia mabadiliko hayo ya kiumiliki hadi pale Simba na Yanga zitakapobadilisha katiba zao kwanza.

Comments

Popular Posts